WCF Kinara katika masuala ya usalama wa afya mahala pa kazi 2021

News Image

Imewekwa: 28th Apr, 2021

WCF YAZOA TUZO KATIKA MAONESHO YA USALAMA NA AFYA MAHALI PA KAZI (OSH 2021)

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umezoa tuzo katika kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya mahali pa kazi duniani baada ya kuibuka kinara wa kundi la Taasisi za bima na Taasisi bora ya Umma inayosimamia vizuri masuala ya usalama na afya mahali pa kazi.

Akikabidhi tuzo hizo wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Wiki ya Usalama na Afya mahali pa kazi duniani yanayofanyika jijini Mwanza kitaifa, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, Mhe. Jenista Mhagama (MB) alitoa rai kwa Mfuko kuendelea kushirikiana na Wakala wa salama na Afya mahali pa kazi (OSHA) ili kuboresha ufanisi katika utendaji kazi.

“WCF endeleeni kushirikiana na OSHA katika programu mbalimbali ili kupunguza ajali, magonjwa na vifo vinavyotokana na kazi. Badilishaneni taarifa za muhimu ambazo zitasaidia kuboresha utendaji wenu kwa sababu mmoja anasimamia mazingira salama ya kufanyia kazi wakati WCF anatoa fidia pale ambapo ajali zimetokea bahati mbaya", alisema Waziri Mhagama na kuongeza;

"Naamini tukifanya haya kwa ushirikiano tutaweza kupunguza madhara makubwa kwa Taifa letu".

Akizungumza baada ya kupokea tuzo hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa WCF Bw. Anselim Peter alisema Mfuko utaendelea kujizatiti katika kuimarisha mifumo inayosimamia usalama na afya kwa wafanyakazi wa Mfuko ili kuhakikisha wafanyakazi wanalindwa na hawawezi kupata madhara yoyote wakiwa katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Tutaendelea kuboresha mazingira yetu kwa kutoa mafunzo na kuwapatia wafanyakazi vitendea kazi muhimu ili kudumisha desturi ya usalama na afya wakati wote”, alisema Bw. Anselim.

Maonesho ya 17 ya Wiki ya usalama na afya Duniani kitaifa yanafanyika jijini Mwanza huku kaulimbiu ikiwa ni ‘Tarajia, jiandae na kabiliana na majanga; Wakati wa kuwekeza katika mifumo madhubuti ya usalama na afya mahali pa kazi ni sasa’.