MAONESHO YA 45 YA KIMATAIFA YA BIASHARA YA DAR ES SALAAM (DITF) 2021

News Image

Imewekwa: 12th Jul, 2021

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (MB) amesema Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) unaendelea kukua kwa kasi ambapo mwaka 2016 ulikuwa na thamani ya bilioni 65.7 na kwa sasa umefikia thamani ya bilioni 438.

Waziri Mhagama aliyasema hayo Julai 5, 2021 wakati alipotembelea banda la WCF kwenye maonesho ya 45 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam viwanja vya Julius Nyerere maarufu Sabasaba ili kujionea jinsi wanachama na wadau wa Mfuko wanavyohudumiwa.

“Mpaka mwaka 2016 malipo ya fidia kwa wafanyakazi walioumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi yalikua kiasi cha shilingo bilioni 1.5, lakini mpaka sasa hivi malipo ya fidia yamefikia shilingi bilioni 27,” alisema Waziri Mhagama na kuongeza;

Waziri Jenista pia alitoa wito kwa waajiri kujisajili na kuwasilisha michango kwa wakati kwa sababu Mfuko una tija kwa kuwa unalinda nguvukazi na kuongeza uzalishaji.

‘Sasa hivi huduma za Mfuko zinapatikana mtandaoni, Mfuko umetengeneza mifumo ya kidijitali kwahiyo waajiri hawana haja ya kutafuta ofisi za Mfuko zilipo”.

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Dkt. John Mduma alisema uwepo wa Mfuko umesaidia kupunguza mzigo kwa waajiri.

“Kuanzishwa kwa Mfuko kumempunguzia mwajiri mzigo ambao alikua nao kipindi cha nyuma lakini kwa sasa mwajiri anabakia na jukumu la uzalishaji huku WCF ikihudumia mfanyakazi aliyepata ajali, ugonjwa au kifo wakati akitekeleza majukumu yake ya kazi”, alisema Dkt Mduma na kutoa wito;

“Nawakaribisha wadau wote ikiwemo waajiri na waajiriwa kutembelea banda letu kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali ikiwemo elimu ya Mfuko na mafao yanayotolewa na namna ya kuwasilisha madai ili wapate haki yao stahiki pindi wanapopata ajali au magonjwa yatokanayo na kazi”.