ILI MFANYAKAZI ALIYEPATA AJALI AWEZE KULIPWA FIDIA LAZIMA TAARIFA YA AJALI ITHIBITISHWE NA POLISI; DKT. MDUMA

News Image

Imewekwa: 24th Jun, 2022

MKURUGENZI Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amesema kwa mujibu wa sheria ili mfanyakazi aliyepata ajali akiwa barabarani aweze kulipwa fidia lazima taarifa ya ajali hiyo ithibitishwe na Jeshi la Polisi.

Dkt. Mduma ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika kikao Kazi baina ya Mfuko, Waajiri na Jeshi la Polisi ikiwa ni mwendelezo wa Mfuko kukutana na makundi mbalimbali (wadau) kwa nia ya kutoa elimu ya Fidia kwa Wafanyakazi.

“Ndio maana sisi kwa pamoja na Jeshi la Polisi tumeona tukutane na waajiri wa Mkoa wa Dar es Salaam na tutaenda na mikoa mingine ili kuwafafanulia umuhimu wa wao kuitafuta hiyo taarifa ya jeshi la polisi mara tu ajali inapotokea,” alifafanua Dkt. Mduma.

Tunasikitika sisi kama Mfuko kuona haki za waajiriwa wanapopata ajali au wategemezi wao zinapotea kwasababu tu taarifa za polisi hazikuwasilishwa kwa maana tukio halikuripotiwa polisi kama ambavyo sheria inataka, alisema Mkurugenzi huyo Mkuu.

Hata hivyo alitoa angalizo kuwa Mfuko unalipa fidia endapo tu ajali hiyo inahusika na mkataba wa kazi anayofanya.

“Kama huyu mwajiriwa amepata ajali wakati akitekeleza jukumu la mwajiri, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi unawajibika kutoa fidia, lakini kama baada ya muda wake wa ajira alikuwa kwenye harakati zake nyingine, itakuwa ni vigumu kwa Mfuko kulipa fidia ya ajali za namna hiyo.” Alisema Dkt. Mduma.

Akijibu baadhi ya hoja za washiriki kuhusu maeneo ya ajali yanayotambulika kisheria, Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter alisema ajali ya barabarani inayotambulika kisheria lazima iwe imetokea kwenye barabara za Umma (public roads) na sio iliyotokea ndani ya makazi ya mtu (residency compound).

Kwaupande wake Afisa Mnadhimu Kikosoi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi, (ACP) Mukada H. Mukadam alisema inapaswa taarifa ya ajali itolewe pindi tu inapotokea na kisheria itolewe ndani ya masaa 72.

“Jukumu letu ni kuthibitisha fomu zinazohusisha ajali zinazotokea barabarani, ni wajibu wako wewe kiongozi kumkumbusha mfanyakazi wako kutoa taarifa polisi na kama hajiwezi kutokana na maumivu ni vema ukatoa taarifa kituo cha polisi na ujiridhishe kama taarifa hiyo imesajiliwa kwenye kitabu cha polisi.” Alifafanua ACP Mukadam.

Tanzania Census 2022