KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU TIXON NZUNDA AWAASA MADAKTARI KUZINGATIA WELEDI NA MAADILI

News Image

Imewekwa: 22nd Feb, 2022

KATIBU MKUU OFISI YA WAZIRI MKUU TIXON NZUNDA AWAASA MADAKTARI KUZINGATIA WELEDI NA MAADILI WANAPOTEKELEZA MAJUKUMU YAO YA KAZI.


KATIBU Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu), Bw. Tixon Nzunda, amewaasa madaktari kuzingatia weledi na maadili wanapofanya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi (impairment assessment of occupational accident and diseases).

Bw. Nzunda ameyasema hayo jijini Mbeya, wakati akifungua mafunzo ya siku tano ya tathmini za ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi (impairment assessment of occupational accident and diseases) kwa madaktari na watoa huduma za afya wapatao 100 kutoka mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Katavi, Rukwa, Songwe, Mbeya, Ruvuma, Njombe na Iringa


“Wakati wote mnapaswa kuzingatia misingi mitatu wakati mkitekeleza majukumu yenu, weledi, uadilifu na uwajibikaji,” alisema Bw. Nzunda.


Alisema kosa lolote dogo (any slight error) litakalofanywa katika kazi ya kufanya tathmini ya ulemavu na magonjwa yatokanayo na kazi litapelekea athari katika maisha ya watu, uchumi wa nchi na kuhujumu Mfuko.


Aidha alisema lengo la Serikali la kuanzisha Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi ni kuhakikisha wafanyakazi wanapata Mafao bora tofauti na sheria ya zamani ya fidia kwa wafanyakazi ili kuboresha fidia.


Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma alisema katika kuhakikisha Mfuko unafanya jukumu lake kubwa la kutoa fidia kwa wale ambao wanapatwa na majanga kutokana na kazini, Mfuko unazingatia kufanya tathmini zinafanyika kwa usahihi na kwa haraka.


“Hili la usahihi lina maanisha tunahitaji kushirikiana na wenzetu hawa ambao tayari ni wataalamu katika maeneo hayo na hili la uharaka lina maanisha Mfuko hauwezi kuwa na madaktari kila kona ya nchi kwa hiyo tunahitaji madaktari ambao wako kwenye vituo mbalimbali ili kushirikiana nasi katika kuhakikiasha swala la tathmini linafanywa kwa haraka na hivyo muhusika anapata fidia stahiki na kwa wakati.” Alifafanua Dkt. Mduma.
Alisema Mfuko utaendelea kufanya kazi zake kwa weledi ndiyo maana unaendelea kuwajengea uwezo wataalamu hao wa afya.


“Kuna miongozo ili kuhakikisha tathmini zinazotolewa na wataalamu hawa zinakuwa na uhakika, zinaaminika na zinatabirika kwa maana kwamba ziko consistent pale ambapo ukifanyiwa tathmini na mtaalamu A na B matokeo yasitofautiane.” Alifafanua.

Dkt. Mduma aliishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu na Serikali kwa ujumla kwa jinsi ambavyo imekuwa ikishirikiana na Mfuko katika kuhakikisha unaendelea kutoa huduma zake kwa ufanisi zaidi