MAAFISA KAZI NCHINI WAASWA KUWA WAADILIFU KATIKA UTEKELEZAJI WA MAJUKUMU YAO

News Image

Imewekwa: 18th Jun, 2022

MAAFISA kazi nchini wameaswa kuwa waadilifu katika utekelezaji wa majukumu yao, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Profesa Jamal Katundu amesema mjini Morogoro Juni 18, 2022 wakati akifungua kikao kazi baina ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na Maafisa Kazi nchini chenye lengo la kuwajengea uelewa wa maboresho ya Sheria ya fidia kwa Wafanyakazi.

Alisema Maafisa Kazi nchini ni mabalozi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, na wanapaswa kuwa na uadilifu wa hali ya juu, WCF ipo Ofisi ya Waziri Mkuu hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao ili kuweka heshima ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

Aidha Kamishna Mkuu Idara ya Kazi Ofisi ya Waziri Mkuu, Bi. Suzan Mgangwa amesema idara yake na WCF zimeazimia kufanya kazi kwa pamoja ili kuendelea kulinda mfanyakazi nchini wanapopata majanga wakati wakitekeleza majukumu yao.

Akizungumza mwanzoni mwa kikao hicho, Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bi. Rifai Mkumba alibainisha kuwa katika muktadha wa kuendelea kuboresha utoaji wa huduma za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi, Bodi imeendelea kusisitiza umuhimu wa Mfuko kuendelea kutoa elimu kwa wadau ikiwa ni pamoja na taasisi mbalimbali hususan za serikali wakiwemo Maafisa Kazi ili kukuza uelewa kuhusu masuala ya fidia ikiwemo huduma mpya kama zilivyoboreshwa na Serikali.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma alisema lengo la kikao kazi hicho ni kujengeana uwezo ili kuwa na uelewa wa pamoja.

“Mabadiliko ya kisera, mabadiliko ya kisheria na kanuni na mabadiliko ya kiutendaji yaliyotokea kwenye mifumo ambayo inatumika kwenye utekelezaji wa shughuli za Mfuko kwa hiyo kikao hicho kitasaidia kuona maendeleo ya mabadiliko hayo.” Alisema Dkt. Mduma.

Tanzania Census 2022