MAONESHO YA NANENANE 2022 YANAAKISI SHUGHULI ZA WCF

News Image

Imewekwa: 4th Aug, 2022

MKURUGENZI wa Huduma za Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. Abdulsalaam Omar, amesema Maonesho ya Nanenane mwaka huu 2022 yanayofanyika jijini Mbeya, yana maana kubwa kwa Mfuko.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar alisema kaulimbiu ya Maonesho hayo inayosema “Agenda 10/30 Kilimo ni Biashara; Shiriki Kuhesabiwa ili kutekeleza vizuri Mipango ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi,” inaakisi moja kwa moja shughuli na mipango ya Mfuko kwa maana hivi sasa kilimo hiki sio kile cha mazoea kwani kinatarajiwa kuweza kuheshimiwa na kuthaminiwa kama ilivyo biashara zingine.

“Kama ulivyosikia siku ile ya ufunguzi wa Maonesho haya, Serikali imedhamiria kukifanya kilimo chetu kuwa cha Biashara, na ndio maana kauli mbiu inataja Kilimo ni Biashara, kwa hivyo hapa unazungumzia ajira za wafanyakazi.” Alisema

Unapozungumzia masuala ya ajira maana yake moja kwa moja WCF inaingia hapo kwa hiyo wote walioajiriwa huko ni wadau wa Mfuko wa Fidai kwa Wafanyakazi na pindi wanapopatwa na changamoto za ajali au magonjwa yanayotokana na kazi wanapokuwa wanatekeleza shughuli zao za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kwa namna moja ama nyingine watastahili kulipwa fidia, alisisitiza Dkt. Omar.

“WCF tuko hapa kukutana na Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili na wao waweze kujua haki zao mbalimbali ni Mafao gani wanaweza wakapata,” alisema.

Alisema kama ambavyo wamekuwa wakitekeleza jukumu la kulipa fidia kwa wafanyakazi wanapougua, au kuumia kutokana na kazi kwa mujibu wa mikataba yao ya kazi, pia wakulima,wafugaji na wavuvi nao watastahili kupata haki za kufaidika na Mafao.

Aliyataja Mafao hayo kuwa ni pamoja na Fao la Matibabu, Fidia ya Ulemavu wa Muda, Mafao ya Ulemavu wa Kudumu na yanaweza kuwa ya mkupuo au kulingana na aina ya ulemavu inaweza kuwa pensheni ya kudumu na endapo itatokea amefariki basi wale wategemezi wake watalipwa fidia na Mfuko.

Kuhusu viwango vya uchangiaji katika Mfuko, Dkt. Omar alisema hivi sasa Serikali imepunguza viwango vya michango kutoka asilimia 0.6% kwenda asilimia 0.5 kwa waajiri walio katika sekta binafsi.

Tanzania Census 2022