MKURUGENZI MKUU WA WCF AKUTANA NA WANUFAIKA WA FIDIA

News Image

Imewekwa: 28th Apr, 2023

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dkt. John Mduma amekutana na wanufaika wa WCF, Bw. Deus Anthony na Bw. Ramadhan Juma kwenye kilele cha siku ya kimataifa ya usalama na afya mahali pa kazi katika viwanja vya Tumbaku mjini Morogoro Aprili 28, 2023.

Wawili hao wamepata ulemavu wa kudumu baada ya kuumia kwa nyakati tofauti wakati wakitekeleza majukumu yao ya kazi.

Bw. Deus Anthony aliumia wakati akishiriki ujenzi wa barabara kati ya Iringa mjini na Igawa ambapo alikatika mguu. Amefaidika na fao la matibabu kutoka WCF hadi alipopona.

“Nilikatika mguu wa kushoto wakati nikiwa kazini mwaka 2017. WCF wamekuwa na mimi kwa kipindi chote cha matibabu hadi kupona na kisha kunipa mguu wa bandia, hivi sasa naweza kutembea bila ya shida yoyote.” Amefafanua Bw. Anthony.

“Nawashukuru sana WCF kwa kuniwezesha kuyamudu maisha, pensheni ninayolipwa kila mwezi kutokana na ulemavu wangu wa kudumu, nimekuwa nikidunduliza na hatimaye nimefanikiwa kumiliki bajaji yangu mwenyewe kutokana na kipato hicho.” Ameongeza kuwa hivi sasa anafikiria kukodi shamba ili alime maharage huko Mikumi.” Amesema

Mnufaika mwingine ni Bw. Ramadhan Juma, ambaye ni mfanyakazi kwenye kiwanda kimoja mjini Kibaha, mkoa wa Pwani. Yeye alikatika mkono wakati akitelekeza majukumu ya kazi akiwa kwenye eneo lake la kazi. Bw. Juma ameelezea jinsi WCF ilivyomuhudumia tangu anauguza jeraha kwenye mkono wake hadi kupona.

“Nilikatika mkono wakati nikiendesha mashine pale kiwandani, nikatibiwa na kupona na baadae WCF wakanipatia mkono wa bandia unaoniwezesha kufanya shughuli mbalimbali.” Alisema mnufaika huyo.

Amesema fidia ya kila mwezi anayolipwa ba WCF imekuwa ikimsaidia katika jukumu la kuhudumia wazazi wake na vilevile wadogo zake.