“NAWASHUKURU WCF KWA KUNIWEZESHA KUYAMUDU MAISHA"- MNUFAIKA WA FIDIA

Imewekwa: 29th Mar, 2023
MNUFAIKA wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Bw. Deus Anthony, ameushukuru Mfuko huo kwa kumuwezesha kuyamudu maisha licha ya kupata Ulemavu wa Kudumu uliotokana na Kazi.
Mnufaika huyo mkazi wa Morogoro ameyasema hayo Aprili 27, 2023 wakati wa Maonesho ya Siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi kwenye viwanja vya Tumbaku mjini Morogoro.
“Nilikatika mguu wa kushoto wakati nikiwa kazini mwaka 2017 na tangu wakati huo, WCF wamekuwa na mimi katika matibabu hadi kupona.”
Amesema hawakuishia hapo “Kwa kuwa nilipata Ulemavu wa Kudumu, WCF wameninunulia mguu wa bandia hivyo naweza kutembea vizuri bila ya shida yoyote,” amefafanua.
Bw. Deus ambaye wakati anaumia kazi yake ilikuwa ni udereva amesema kwa kutumia pensheni ya kila mwezi anayolipwa na WCF ameweza kununua bajaji baada ya kudunduliza.
“Nawashukuru WCF kwa kuniwezesha kuyamudu maisha, hivi sasa nafikiria kukodi shamba ili nilime maaharage huko Mikumi.” Amesema
Kuhusu ushiriki wa WCF kwenye Maonesho hayo yaliyofanyika kitaifa mjini Morogoro, Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar amesema pamoja na kulipa fidia Mfuko unalo jukumu la kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi lakini pia kutoa elimu kwa Umma;
“Na hapa ni mahali sahihi, kwani tunakutana na wananchi na wafanyakazi lakini pia tunakutana na waajiri, hivyo hii ni fursa nzuri kwetu na kwa wadau wetu pia.” Alisema Dkt. Omar.
Alisema katika banda la WCF wanatoa Elimu ya Fidia kwa njia mbalimbali ikiwemo michoro inayoonyesha tofauti ya viwango vya Ulemavu vinavyotumika katika kulipa fidia.
Aidha Meneja Tathmini za vihatarishi vya Usalama mahali pa kazi WCF, Bi. Naanjela Msangi amesema wanatoa Elimu kwa nadharia lakini pia kuna vifaa mbalimbali vya kujihami dhidi ya majanga kazini vya kusaidia kutoa elimu.
“Tunaonyesha vifaa sahihi vya kujihami kama vile mask (N95) kuzuia vumbi (normal dust), mask za kuzuia vumbi lenye kemikali kikiwa full face, Kifaa cha kupima viwango vya kelele maeneo ya kazi, kupima viwango vya mitetemo mwili mzima na mikono, kifaa cha kukinga kelele (ear muff), safety boots, reflectors, overalls na hand gloves." alifafanua.
Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi hufanyika Aprili 28 kila mwaka ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuiadhimisha siku hiyo, lengo kubwa ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za wafanyakazi katika sehemu za kazi. Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka 2023 ni “Mazingira salama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.”.