TEMEKE ONE STOP JAWABU

News Image

Imewekwa: 25th Sep, 2020

MKUU WA MKOA WA DAR ES SALAAM AUPONGEZA MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI KWA KUTOA ELIMU KUSIKILIZA NA KUTATUA KERO ZA WAAJIRI NA WAAJIRIWA.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Abubakar Kunenge ameupongeza Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) katika ushiriki wake wa kusikiliza na kutatua kero na changamoto za wadau wa Mkoa wa Dar es Salaam na nchini kwa ujumla.

Akizungumza baada ya kutembelea banda la WCF katika jukwaa la Temeke One Stop Jawabu linaloendelea katika viwanja vya MwembeYanga alisema, "Uwepo wa Mfuko katika viwanja hivi umesaidia sana wananchi wa Dar es Salaam hasa wilaya ya Temeke na maeneo ya jirani kama Mkuranga, Kisarawe ambao walikua na changamoto za madai, usajili, elimu pamoja na masuala mbalimbali yanayohusu fidia kwa wafanyakazi".

Mhe. Kunenge aliongeza kuwa uwepo wa Mfuko katika viwanja hivi utasaidia wananchi kupata haki zao za fidia kama sheria inavyoelekeza.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Godwin Gondwe alitoa rai kwa Mfuko kuendelea kutoa elimu kwa wadau wake ili kuhakikisha wanawafikia wadau wengi nchini, "Mfuko unafanya kazi kubwa sana hasa katika kuwalinda wafanyakazi ambao wanapata majanga kazini na wadau wengi bado hawajui cha kufanya wanapopata ajali, magonjwa au kifo kutokana na kazi, nawaomba muendelee kutoa elimu kwa waajiri na waajiriwa wote ili tuendelee kuunga mkono juhudi za Mhe. Rais kuelekea uchumi wa viwanda".

Jukwaa la Temeke One Stop Jawabu ni kampeni iliyoanza tarehe 14 hadi 28 Septemba 2020 ambayo inajumuisha Taasisi mbalimbali za Umma na binafsi zilizokusanyika kwa ajili ya kuwahudumia na kutatua kero za wanaTemeke. WCF inashiriki ambapo wadau mbalimbali wanafika kwa ajili ya kufuatilia madai, michango, usajili pamoja na kupata elimu ya fidia kwa wafanyakazi.