Uchangiaji sekta binafsi sasa ni asilimia 0.6 badala ya asilimia 1

News Image

Imewekwa: 26th Jul, 2021

SERIKALI YASHUSHA KIWANGO CHA MICHANGO YA WAFANYAKAZI KATIKA SEKTA BINAFSI KUTOKA ASILIMIA 1% MPAKA ASILIMIA 0.6%

SERIKALI kupitia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) imeshusha viwango vya uchangiaji kwenye Mfuko huo ambapo sasa Waajiri kutoka Sekta Binafsi watachangia asilimia 0.6 ya mishahara ya wafanyakazi wao kutoka asilimia 1 waliyokuwa wakichangia hapo kabla.

Akitangaza uamuzi huo wa serikali, mbele ya waandishi wa habari kwenye Makao Makuu ya Mfuko huo jijini Dar es Salam leo Julai 26, 2021, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma alisema waajiri wote kutoka sekta binafsi wataanza kuchangia kiwango hicho kipya cha asilimia 0.6 ya mshahara wa mfanyakazi kuanzia mwezi huu wa Julai, 2021.

Alisema lengo la mabadiliko hayo ya kiwango cha uchangiaji ni kumpunguzia mzigo mwajiri ili fedha alizokuwa akitumia kuchangia sasa aelekekeze fedha hizo kwenye maeneo mengine ya uendeshaji wa shughuli zake za uzalishaji.

ā€œ Uamuzi huu ni utekelezaji wa maelekezo ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassani,amekuwa akitoa kuhusu Taasisi za Serikali kuhakikisha zinaweka mazingira bora ya ufanyaji biashara na uwekezaji nchini ili kukuza uchumi wa Nchi na kulinda Rasilimali Watuā€ Alisema.

Aliwahakikishia waajiri na waajiriwa kuwa licha ya punguzo hilo, Mafao yanayotolewa na Mfuko yatabaki kama yalivyo kama ambavyo sheria iliyoanzisha Mfuko ya mwaka 2016 inavyosema.

ā€œ Tuliona hili liwekwe bayana isije kuonekana kwamba kwa kupunguza kiwango cha uchangiaji basi huenda na Mafao nayo yatapungua, la hasha Mafao yatabaki kama yalivyo kwani tumejihakikishia kwa kushirikiana na wataalamu kuwa kwa kufanya hivyo Mfuko utabaki imara na kuwa endelevu.ā€ Alisisitiza.

Aidha Dkt. Mduma alisema mchakato huo umepitia sehemu mbalimbali na kutoa shukrani kwa Chama Cha Waajiri nchini (ATE) na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) kwa kushirikiana na Mfuko kiekie kajia jumbo Hilo.

Pomoja na mambo mengine alisema kuanzia Julai mwaka huu serikali imeshusha viwango vya uchangiaji kwenye Mfuko ambapo sasa Waajiri kutoka Sekta Binafsi watachangia asilimia 0.6% ya mishahara ya wafanyakazi wao kutoka asilimia 1% waliyokuwa wakichangia hapo zamani wakati waajiri kutoka sekta ya Umma wao wataendelea kuchangia asilimia 0.5% kama ilivyokuwa hapo awali.