UJUMBE WA KAMATI YA KUDUMU YA SHERIA NDOGO YA BARAZA LA WAWAKILISHI YATEMBELEA WCF

News Image

Imewekwa: 12th Oct, 2022

UJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo ya Baraza la Wawakilishi ukiongozwa na mwenyekiti wake, Mhe. Mihayo Juma Nunga umetembelea ofisi za Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) jijini Dar es Salaam Oktoba 12, 2022 kwa nia ya kujifunza.

Akizungumza baada ya kukutana na Watendaji wa Mfuko huo wakiongozwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, mwenyekiti huyo alisema, ziara hiyo imewawezesha kupata uelewa mpana wa namna Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi inavyotekelezwa.

“Kwetu jambo hili ni geni halijatengenezewa utaratibu mzuri na sahihi wa kuwalipa fidia wafanyakazi waliopata changamoto kwenye maeneo ya kazi, Zanzibar tuko katika maandalizi ya kutengeneza utaratibu wa jinsi gani Mfanyakazi atapata fidia pindi anapoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, kwahivyo tukaona tutembelee Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ambao wana uzoefu mkubwa katika masuala haya.” Alifafanua Mhe. Nunga.

Alisema wameona jinsi watu wengi walivyonufaika na uwepo wa WCF kwa hivyo ni wakati muafaka kwa Zanzibar kuwa na Mfuko utakaotoa huduma bora kama ambavyo wameshuhudia hapo WCF.

Naye Mkurugenzi Mwendeshaji wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), Bw.Ali Nassor Shaaban, alisema Mfuko huo uko katika maandalizi ya kuanzisha huduma hiyo ya kulipa fidia wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

“Tumeona kabla ya kuanzisha chombo hicho ni vema kujifunza kwa wenzetu WCF ili kujua sheria na kanuni zake zilivyo ili tuwe katika nafasi nzuri ya kuanzisha chombo chetu kitakachotoa huduma kulingana na mazingira ya Zanzibar.” Alifafanua.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Dtk. John Mduma alisema, WCF ina uzoefu wa mika saba (7) katika masuala ya utoajifidia kwa wafanyakazi na imekuwa ni wakati mzuri wa kubadilishana mawazo namna bora ya kuendesha vyombo hivi vya Fidia kwa Wafanyakazi.

“Tumewaeleza namna tunavyotenda katika miaka hii saba (7) na tumejifunza mambo mengi ambayo wamekuwa wakituuliza na tunaamini wamejifunza mengi.” Alifafanua.