UTENDAJI BORA WA WCF WAPONGEZWA NA UJUMBE WA WIZARA YA KAZI KENYA

News Image

Imewekwa: 25th Apr, 2023

UJUMBE kutoka Wizara ya Kazi nchini Kenya ukiongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Bw. Geoffrey Kaituko umetembelea Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) na kusema “umekunwa” na utendaji bora wa WCF na kuuita kuwa ni Kinara katika masuala ya Fidia kwa Wafanyakazi barani Afrika.

Ziara ya Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Kazi kwenye ofisi za WCF imekuja ikiwa ni mwaka mmoja tu baada ya Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi nchini Kenya (DOSHS), Dkt. Musa Nyandusi akifuatana na maafisa kadhaa kutembelea WCF kwa nia ya kujifunza masuala ya fidia kwa wafanyakazi.

“Tanzania ni nchi ambayo ina taasisi nzuri kwenye sekta ya Kazi. Wakati mwingine watu hupenda kwenda Ulaya kujifunza mambo ambayo kumbe yanapatikana hapa Afrika. Sisi tunawashukuru sana kwa kutupatia nafasi hii.” Alisema Katibu Mkuu huyo Bw. Geoffrey Kaituko.

Aidha Mkurugenzi wa DOSHS nchini Kenya, Dkt. Musa Nyandusi ameuelezea Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kama kinara Afrika kutokana na mfumo wake wa kulipa fidia.

“Tumejifunza mengi kutoka kwenu na tunaendelea kujifunza” tunawashukuru na tunawasihi msituchoke kwani ninyi mmeshatangulia kwenye barabara hii hakuna haja ya sisi kujikwaa wakati ninyi mnajua wapi ni vigumu kupita na hivyo mtatuelekeza ili nasi tuweze kuwa na chombo kama hiki cha kuwatumikia wananchi wetu.” Alisema Dkt. Musa Nyandusi.

Akiwakaribisha kwenye ofisi za WCF, Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini WCF, Bw. Emmanuel Humba alisema licha ya kwamba WCF ina umri mdogo tangu kuanzishwa kwake tayari imefanya mambo makubwa katika kuhakikisha nguvu kazi ya Watanzania inalindwa kwa kulipa fidia stahiki pindi Mfanyakazi anapoumia ama kuugua kutokana na kazi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uendeshaji WCF, Bw. Anselim Peter ambaye alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu Dkt. John Mduma alisema Mfuko umekuwa ukipiga hatua kubwa katika utoaji wa huduma zake na kwamba hivi sasa kwa asilimia kubwa huduma za Mfuko zinatolewa kupitia TEHAMA.