WAKULIMA, WAFUGAJI NA WAVUVI WALIO KATIKA AJIRA NI WATEJA WETU-WCF

News Image

Imewekwa: 7th Aug, 2022

MKURUGENZI wa Huduma za Tathmini, Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) Dkt. Abdulsalaam Omar, amesema Maonesho ya Nanenane mwaka huu 2022 yanayofanyika jijini Mbeya, yana maana kubwa kwa Mfuko huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko huo alisema kaulimbiu ya Maonesho hayo inayosema “Agenda 10/30 Kilimo ni Biashara; Shiriki Kuhesabiwa ili kutekeleza vizuri Mipango ya Kilimo, Ufugaji na Uvuvi,” inaakisi moja kwa moja shughuli na mipango ya WCF kwa maana hivi sasa kilimo hiki sio kile cha mazoea kwani kinatarajiwa kuongeza ubora na kuthaminiwa kama ilivyo biashara zingine hili ni jambo kubwa la kukuza uchumi wa nchi nasisi WCF tunaipongeza sana Serikali ya Awamu ya sita, inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kama ulivyosikia siku ile ya ufunguzi wa Maonesho haya, Serikali imedhamiria kukifanya kilimo chetu kuwa cha Biashara, na ndio maana kauli mbiu inataja Kilimo ni Biashara, kwa hivyo hapa unazungumzia ajira za wafanyakazi.” Alisema

Unapozungumzia masuala ya ajira maana yake moja kwa moja WCF inaingia hapo kwa hiyo wote walioajiriwa rasmi ni wadau wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na pindi wanapopatwa na changamoto za ajali au magonjwa yanayotokana na kazi wanapokuwa wanatekeleza shughuli zao za Kilimo, Ufugaji na Uvuvi kwa namna moja ama nyingine watastahili kulipwa fidia, alisisitiza Dkt. Omar.

“WCF tuko hapa kukutana na Wakulima, Wafugaji na Wavuvi ili na wao waweze kujua haki zao mbalimbali ikiwemo ni Mafao gani wanaweza wakapata na tunawakaribisha wananchi katika Banda la WCF.”alisema.

Alisema kama ambavyo wamekuwa wakitekeleza jukumu la kulipa fidia kwa wafanyakazi wanapoumia au kuugua kutokana na kazi kwa mujibu wa mikataba yao ya kazi, pia wakulima,wafugaji na wavuvi nao watastahili kupata haki za kufaidika na Mafao hayo kwa vigezo vile vile vinavyotumika.

Aliyataja Mafao hayo kuwa ni pamoja na Fao la Matibabu, Fidia ya Ulemavu wa Muda, Mafao ya Ulemavu wa Kudumu na yanaweza kuwa ya mkupuo au kulingana na kiwango inaweza kuwa pensheni ya kila mwezi, naendapo itatokea amefariki basi wale wategemezi wake watalipwa fidia na Mfuko.

Kuhusu viwango vya uchangiaji katika Mfuko, Dkt. Omar alisema hivi sasaSerikali imepunguza viwango vya michango kutoka asilimia 0.6% kwenda asilimia 0.5 kwa waajiri walio katika sekta binafsi sawa na wale wa sekta ya Umma.

Wakizungumza baada ya kutembelea banda la WCF, wafanyakazi mbalimbali wameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wake Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuuwezesha Mfuko huo kuwahudumia wafanyakazi wanapopatwa na changamoto mbalimbali wawapo kazini.

“Ni jambo jema sana Mfanyakazi anapokuwa anatekeleza majukumu yake na ikatokea amepata changamoto za kuumia, kuugua ama kufariki akiwa kazini aweze kupata haki yake ya kufidiwa, ni kitu kizuri na ninampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuuwezesha Mfuko huu kutekeleza majukumu yake.” Alisema Bw. John Chazi ambaye ni Mfanyakazi kwenye Chuo Cha Kilimo Inyala, Mbeya.

Mfanyakazi mwingine wa jijini Mbeya Bw. Aloyce Gonzaga alisema yeye amepata Elimu zaidi kwani alikuwa anausikia Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi na aliamua kutembelea banda la WCF ili kupata uelewa zaidi wa namna gani mfanyakazi anaweza kufidiwa endapo atapata madhila yoyote akiwa kazini.

Aidha Afisa Mfawidhi wa WCF Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bi. Rose Satta ametoa wito kwa wafanyakazi kutoka sekta zote walio katika ajira rasmi kwenye Kanda hiyo kutembelea Ofisi za WCF Kanda zilizoko jijini Mbeya.