WAZIRI MHAGAMA AZINDUA BODI YA WADHAMINI YA MFUKO WA FIDIA KWA WAFANYAKAZI (WCF)

News Image

Imewekwa: 4th Oct, 2021

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Joachim Mhagama (MB), ameitaka Bodi mpya ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) kulinda mafanikio makubwa yaliyopatikana kutokana na uwepo wake kwa wivu na nguvu zote.
Mhe. Mhagama ameyasema hayo wakati akizindua Bodi hiyo chini ya Mwenyekiti wake Bw. Emanuel Humba kwenye hafla fupi iliyofanyika katika ukumbi wa mikutano Magadu mkoani Morogoro.
“ Kumekuwa na Mafanikio makubwa ya Mfuko katika kipindi hiki cha miaka sita tangu uanzishwe na mnatakiwa kuyalinda kwa wivu na kwa nguvu zenu zote.” Alifafanua na kutoa mfano………katika kipindi ambacho bodi haikuwepo, thamani ya Mfuko imekuwa hadi kufikia shilingi za Kitanzania bilioni 445.49 kutoka thamani ya Mfuko ya shilingi bilioni 112.83 mwaka 2016/2017, huu ni ukuaji mkubwa sana na tunaona kuna kazi kubwa imefanyika, lindeni mafanikio haya.” Alisisitiza.
Mafanikio mengine Mhe. Mhagama alisema “Hata katika ulipaji wa Mafao, kufikia mwaka 2020/2021 Mfuko ulilipa Mafao ya Wafanyakazi waliopata ajali kazini shilingi bilioni 12.43 ikilinganishwa na mwaka 2016/2017 ambapo zililipwa shilingi bilioni 1.55 tu.
Aidha aliwaasa Wajumbe wa Bodi kuelewa vema lengo la uwepo wa Mfuko ambapo ni kuhakikisha Wafanyakazi wanaoumia, Kuugua ama Kufariki kutokana na Kazi zao kwa mujibu wa Mikataba ya Ajira zao basi Serikali kupitia WCF iwalipe fidia au iwatibu na wakipona warejee kazini kuendelea na majukumu yao.
Aliwakumbusha kuhusu kuyaelewa vema majukumu yao kama yalivyoanishwa kisheria katika kifungu cha 13, 14, 15 na 16, na sehemu ya majukumu hayo ni pamoja na kusimamia maslahi ya wafanyakazi yanayotokana na kuanzishwa kwa sheria ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Mhe. Jenista Mhagama almpongeza Mwenyekiti huyo wa Bodi Bw. Humba kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo kwa kipindi cha pili na pia amewapongeza Wajumbe wa Bodi aliowateua na kuwataka waende kuusimamia Mfuko kwa kushirikiana na Menejimenti ili kufikia matarajio ya Serikali.
Wajumbe wa Bodi walioteuliwa na Mhe. Waziri Jenista Mhagama ni pamoja na Onorius John Njole, Perfect Raphael Kilenza, Ibrahim Barnabas Mahumi, Abdulaziz Alladin Shambe, Rifai A. Mkumba, Raymond Kaseko, Juliana C.N. Mpanduji, Rehema Rashid Ludanga na Felix Kagisa Rugarabamu.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Emanuael Humba alimuhakikishia Mheshimiwa Waziri Mhagama kuwa watahakikisha Mfuko unaendelea kutekeleza majukumu yake kulingana na malengo ya Mfuko na matarajio ya Serikali.
“Mashirika mengi yanakufa kutokana na kujisahau kwa waliopewa dhamana ya kusimamiwa mashirika haya, sisi ni wadhamini tu, na kwahiyo udhamini wetu lazima tuulinde kwa hali na mali kwa kutenda haki.” Alisema Bw. Humba.Bw. Humba alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini kuongoza Bodi hiyo na kutoa hakikisho ya kufanya kazi kwa uwezo wake wote.
“Naomba wajumbe wenzangu tuutendee haki uaminifu ambao Mheshimiwa Rais na Mheshimiwa Rais wametupatia kwa kufanya kazi kwa Weledi na bidii kwa hiyo nawaombeni tutende haki.” Alibainisha.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma alimpongeza Mwenyekiti wa Bodi Bw. Emmanuel Humba na Wajumbe wote kwa kuaminiwa kupewa dhamana hiyo ili kuendesha gurudumu la Mfuko.
Lakini pia alitoa pongezi kwa Mhe. Waziri Mhagama kwa kuteua wajumbe kwa kuzingatia kubakia kumbukumbu ya Taasisi kwa kuwabakisha wachache waliokuwepo katika Bodi ya wali na kuteua wengine wapya hali itakayosaidia kuufikisha Mfuko mahala panapostahili.
Akizungumza kwa niaba ya Chama cha Waajiri Nchini (ATE), Mkurugenzi Mkuu, Suzana Ndomba alisema WCF ni muhimu kwa Waajiri, Wafanyakazi na Jamii nzima na mafanikio ya Mwajiri hutegemea Mfanyakazi.
“Kutokana na tathmini iliyofanywa na Serikali kuwa Mfuko utakuwa endelevu kwa miaka 30 ijayo Waajiri tunaamini katika utendaji wa Mfuko na tutaendelea kushirikiana na Mfuko ili kuuwezesha kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sharia.” Alisema Ndomba.
Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Nchini (TUCTA), Tumaini Nyamhokya yeye alifurahishwa na viwango vya Fidia inayotolewa ukilinganisha na ile iliyokuwa ikitolewa kabla ya mabadiliko ya Sheria yaliyoanzisha WCF.
“Kipindi cha nyuma kulikuwa na shida sharia ilikuwa ngumu mfanyakazi akiumia mwisho wa malipo ni shilingi 108,000/= ambayo ndiyo kiwango cha juu, lakini bahati nzuri viongozi tulilalamika na hatimaye sharia ilibadilika na sasa hivi mfanyakazi anapoumia analipwa kulingana na percentage ya uumiaji, kwen=tu sisi imetuweka katika mazingira mazuri na tunaishukuru Serikali kwa kuliona hilo.” Alisema Nyamhokya.