WCF YAPATA TUZO SABASABA 2021

News Image

Imewekwa: 20th Jul, 2021

WCF YAPATA TUZO SABASABA 2021

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umepongezwa kwa kuibuka mshindi wa pili katika kundi la Taasisi za Bima na Hifadhi ya Jamii zilizoshiriki kwenye Maonesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba yaliyofanyika katika viwanja vya Mwl. Nyerere jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya hafla ya ufungaji wa maonesho hayo, mmoja wa wadau ameeleza kuwa ushindi huo ni chachu kwa Mfuko kuendelea kutoa huduma nzuri kwa wadau wake ikiwemo kujitangaza kupitia maonesho na makongamano yanayohusisha wadau tofauti nchini.

“Nawapongeza sana WCF kwa kuibuka washindi wa pili, binafsi niliposikia wapo sabasaba nilisema ni lazima niwatembelee, na kwa kweli wamenihudumia vizuri sana. Ninashauri wasiishie kushiriki sabasaba tu, waendelee kujitangaza kupitia makongamano ya wadau, alisema Athuman Saidi, mmoja ya waliotembelea maonesho hayo.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma, baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo amesema ushindi huo umezidi kuwapa motisha zaidi kuendelea kutoa huduma za fidia stahiki kwa wakati pamoja na elimu ya taratibu za madai ili kuepukana na vikwazo vinavyochangia Mfanyakazi kukosa sifa ya kulipwa fidia yake. Ameahidi kufanyia kazi maoni yaliyowasilishwa na wadau waliotembelea banda la Mfuko huo kwa lengo la kuendelea kuwa mfano wa kuigwa barani Afrika katika utoaji wa huduma za fidia.

"Katika maonesho haya tumekuwa washindi wa pili kwetu ni wajibu mkubwa tumepewa katika kuonesha tofauti kati ya mshindi na asiyeshinda lakini zaidi ushindi huu unapaswa kuwa na tija katika utoaji wa huduma za fidia ili kuendelea kuwa mfano wa kuigwa," amefafanua.

Tuzo hiyo ilitolewa na Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla wakati wa sherehe za kufunga maonesho hayo zilizoenda sanjari na utoaji wa zawadi kwa washindi wa makundi mbalimbali.

Katika Maonesho ya 45 kundi la Bima na Taasisi za Hifadhi ya jamii lilijumuisha taasisi za Bima na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ambapo maboresho makubwa yaliyochangia WCF kupata ushindi kwa mwaka huu ilikuwa ni pamoja na kutekeleza mapendekezo ya wadau wa sekta binafsi ya punguzo la viwango vya uchangiaji pamoja na kuimarisha matumizi ya huduma za kimtandao katika utoaji wa huduma za Fidia.

Maonesho haya yalifunguliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango mnamo Julai 5, 2021 ambapo nchi mbalimbali zilishiriki maonesho ya mwaka huu ikiwemo China, Umoja wa Falme za Nchi za Kiarabu (UAE), Marekani na Uturuki.