WCF IMELIPA FIDIA SHILINGI BILIONI 65.4 KUFIKIA SEPTEMBA 2023-DKT. MDUMA

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umeshalipa fidia kiasi cha shilingi bilioni 65.4 hadi kufikia Septemba, 2023.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, wakati akitoa wasilisho lake katika kikao kazi na Wahariri wa vyombo vya habari, kuelezea utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya WCF, miaka 8 tangu kuanzishwa kwake.
Sambamba na hilo pia amesema Mfuko umeweza kusajili asilimia 95% ya waajiri wote wanaostahili kujisajili na Mfuko na kuahidi kuwa Mfuko uko mbioni kukamilisha asilimia 5% ya waajiri ambao bado hawajajisajili na Mfuko.
Mafanikio mengine ameyataja kuwa ni pamoja na kupanuka kwa wigo wa utoaji huduma kwa kuingia makubaliano na hospitali, watoa huduma mbalimbali za afya nchini na ufunguzi wa ofisi mikoani.
Pia aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kuboreshwa kwa huduma kupitia usimikaji mifumo ya TEHAMA, kuboreshwa kwa kituo cha huduma kwa wateja (Call Centre) na kuboreshwa kwa tathmini za ulemavu kupitia mafunzo kwa madaktari sehemu mbalimbali nchini.
Akieleza zaidi alisema, hadi kufikia Septemba 2023, thamani ya Mfuko imefikia bilioni 697.5
Alisema jambo jema ni kwamba Mfuko kuwa na uwezo endelevu wa kulipa fidia mpaka mwaka wa fedha 2047/2048 kulingana na tathmini ya uhai na uendelevu wa Mfuko ya mwaka 2018, ambayo ilifanywa na Shirika la Kazi Duniani ILO.
“WCF imefanya tathmini ya pili mwaka 2022 ambayo imeonesha kuwa Mfuko ni himilivu na unauwezo wa kuendelea kutoa huduma bila kutetereka.” Alisisitiza Dkt. Mduma.
Alisema WCF sio tu inalinda nguvu kazi ya taifa lakini pia waajiri sasa wana muda mrefu wa kuendelea na kazi za uzalishaji huku jukumu la kumuhudumia mfanyakazi aliyeumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi likibebwa na WCF.
“Lakini pia uwepo wa WCF umeleta tija kazini kutokana na mahusiano mazuri kati ya waajiri na waajiriwa, lakini pia kupunguza umaskini hususan kwa wategemezi na wafanyakazi wanaopata ulemavu wa kudumu na kushindwa kurudi kazini au kufariki.” Alisema.
Alisema Mfuko unachangia ongezeko la uzalishaji na maendeleo ya Taifa kupitia ongezeko la tija, ongezeko la pato la taifa na kodi ili kuiwezesha Serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi
Dkt. Mduma pia alisema, kutokana na mafanikio ambayo Mfuko umeyapata, umekuwa kinara na umeweza kuwafanya majirani toka nchi za Zambia, Kenya, Botswana, Afrika Kusini na Zimbabwe kujifunza kutoka WCF.
Akizungumzia majukumu ya WCF, Dkt. Mduma alisema, ni pamoja na Kusajili Waajiri waliopo katika Sekta ya Umma na Binafsi Tanzania Bara, Kukusanya michango kutoka kwa Waajiri, Kulipa Fidia kwa Mfanyakazi atakayeumia, kuugua ama kufariki wakati akitekeleza majukumu ya mwajiri wake.
Majukumu mengine alitaja kuwa ni Kutunza kumbukumbu za matukio ya ajali, magonjwa na vifo kutokana na kazi, Kukuza mbinu za kuzuia ajali, magojwa na vifo kutokana na kazi na Kuelimisha Umma kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi.
Kwa upande wake, Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR) ambayo ndiyo yenye jukumu la kusimamia utendaji wa Mashirika yote ya Umma, imeweka utaratibu kwa viongozi wa taasisi hizo kukutana na wahariri na waandishi wa habari ili kuueleza umma wa Watanzania mambo ambayo taasisi hizo zinatekeleza.
Chini ya utaratibu huo WCF inakuwa ni taasisi ya 11 kukutana na wahariri na waandishi wa habari nchini.
“Kwa mantiki hiyo Ofisi ya Msajili wa Hazina ikaona umuhimu na msingi wa kuzikutanisha taasisi za umma na umma wenyewe kupitia vyombo vya habari.” Alisema Bw. Thobias Makoba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Ofisi ya Msajili wa Hazina (TR)
Alisema, malengo sio tu kutoa elimu lakini iwe ufunguo kwa taasisi kufanya muendelezo wa kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya habari.
Akifafanua zaidi alisema, Msajili wa Hazina (TR) alielekeza mara kadhaa kwa taasisi za umma kila zinapoandaa taarifa za fedha za kila mwaka wahakikishe zinatangazwa ili umma ujue mwenendo wa mashirika yao.
"Umma ukiwa na uelewa wa kutosha itakuwa rahisi kwao kubaini usahihi wa kinachoelezwa kuhusu taasisi fulani." Alisema Bw. Makoba.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Bw. Deodatus Balile, ameishukuru ofisi ya Msajili wa Hazina kwa kuandaa utaratibu wa wakuu wa taasisi kukutana na vyombo vya habari.
“Lakini hapa nataka niwaambie ninyi wahariri na hawa ndugu zetu wanaofaidika na fidia, muwe mabalozi wa Mfuko huko muendako ili watanzania wengi zaidi waweze kufaidika na huduma za WCF.” Alisema.