WCF KUSAJILI WAAJIRI WOTE NCHINI

News Image

Imewekwa: 20th Oct, 2023

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Mhandisi Cyprian Luhemeja, ametoa maagizo manne kwa Baraza la wafanyakazi la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) ikiwamo kuwasajili waajiri wote nchini.

Mhandisi Luhemeja, ameyasema hayo Oktoba 19, 2023 mkoani Morogoro, alipokuwa akifungua kikao cha Baraza hilo.

Amesema ni muhimu WCF ikaongeza malengo ya kusajili waajiri wote hasa wa sekta binafsi ambao wanaajiri wafanyakazi wengi wa ngazi ya chini na wanaofanya kazi kwenye mazingira hatarishi.

“Suala jingine ni elimu kwa umma huu mfuko ni muhimu, unawagusa watanzania wote kutokana na wapendwa wao kupata madhila kazini, wajue manufaa ya mfuko na majukumu yake,”amesema.

Pia, amehimiza kuwa wabunifu katika kutekeleza majukumu ili watanzania wavutiwe na huduma zinazotolewa.

Naye, Mwenyekiti wa baraza hilo ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma, amesema mfuko upo imara na wajumbe wa baraza hilo wamejadili masuala mbalimbali ikiwamo huduma za utengamao.