WCF YATOA ELIMU YA FIDIA KWA WAFANYAKAZI MAONESHO YA MADINI RUANGWA

News Image

Imewekwa: 29th Aug, 2023

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umetumia fursa ya Maonesho ya Madini wilayani Ruangwa mkoani Lindi yaliyofikia kilele Agosti 26, 2023, kukutana na wadau na kutoa elimu ya fidia kwa wafanyakazi.

Sekta ya madini ni miongoni mwa maeneo yanayotoa ajira kwa watanzania wengi ambao kwa mujibu wa sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, mwajiri anapaswa kujisajili na Mfuko na kuwasilisha michango kila mwezi na endapo mfanyakazi ataumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi, ni wajibu wa WCF kumlipa fidia.

Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), imeutaja Mkoa wa Lindi kuwa na Madini Mkakati sita ambayo ni Chuma, Kinywe, Dhahabu, Shaba, Magnesite, pamoja na Madini Muhimu manne ambayo ni Jasi, Chokaa, Chumvi na Chuma hali inayoonyesha kuwa ajira nyingi zitokanazo na upatikanaji wa madini hayo zitazalishwa.

Aidha afisa Madini Mkazi Mkoa wa Lindi Mhandisi Iddi Msikozi, amesema Maonesho hayo yaliwaleta pamoja wadau wa sekta hiyo kutoka nchi zaidi ya 10 duniani na lengo lilikuwa ni kuonesha dunia kwamba Tanzania imebarikiwa kuwa na rasilimali Madini za kutosha na wadau wamekaribishwa kuwekeza katika mkoa huo ili Watanzania wanufaike na uchumi wa madini.

Dhima ya WCF ni kupunguza athari za kijamii na kiuchumi za majanga yatokanayo na kazi kwa wafanyakazi, familia zao na waajiri kwa kutoa fidia stahiki, kwa usawa, uendelevu na ufanisi.

Ushiriki huo wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi katika Maonsho hayo ni utekelezaji wa moja ya majukumu ya Mfuko ya Kukuza mbinu za kuzuia ajali, magonjwa ama vifo vinavyotokana na kazi kwa kutoa elimu kwa Umma na wadau wa Mfuko.