WCF YATWAA TUZO YA UBORA KATIKA FIDIA NA BIMA ZA WAFANYAKAZI

News Image

Imewekwa: 30th Apr, 2023

MFUKO wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umetwaa tuzo ya “Best OSH Policy for Workers in Insurance Services” wakati wa kilele cha Siku ya Kimataifa ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi 2023 kwenye viwanja vya Tumbaku mjini Morogoro.

Kauli mbiu ya maadhimisho kwa mwaka 2023 ambapo mgeni rasmi alikuwa ni alikuwa ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Profesa Joyce Ndalichako.

“Mazingira salama na afya ni kanuni na haki ya msingi mahali pa kazi.”.

Kilele cha Maadhimisho ya siku ya Kimataifa ya Usalama na Afya mahali pa kazi hufanyika Aprili 28 kila mwaka ambapo Tanzania huungana na mataifa mengine duniani kuiadhimisha siku hii, lengo kubwa ni kuendeleza kampeni za kuhamasisha uwepo wa mazingira salama na yenye kulinda afya za watu katika sehemu za kazi.

Akipokea tuzo hiyo Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema tuzo hiyo ni faraja kwa Wafanyakazi wa WCF na itachochea kuongeza umakini wa kuzidi kuwa Madhubuti katika mifumo ya kudhibiti ajali na magonjwa mahali pa kazi.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tathmini wa WCF, Dkt. Abdulsalaam Omar amesema “Hii inatupa matumaini na hamasa ya kuendelea kuboresha maeneo ya kazi na kwakuwa WCF ni mdau mkubwa katika masuala haya hatuishii kwa wafanyakazi wetu pekee bali hata kwa wafanyakazi wengine ambao ni wadau wa WCF.”