WCF YAWANOA WAAJIRI MKOANI MWANZA JUU YA UTOAJI WA TAARIFA SAHIHI

News Image

Imewekwa: 21st Jun, 2022

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) umetoa semina kwa Waajiri mkoani Mwanza, kwa lengo la kutoa elimu ya kuwajengea uelewa kuhusu umuhimu wa taarifa za polisi katika ulipaji wa fidia.

Semina hiyo imefanyika Jumanne Juni 21, 2022 katika ukumbi wa Chuo cha Fedha (IFM) kampasi ya Mwanza uliopo kwenye jengo la Rock City Mall jijini Mwanza.

Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Bw. Anselim Peter ambaye ni Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi alisema kuwa, kuwajengea uelewa waajiri itapunguza changamoto ya madai ya fidia kwa wafanyakazi katika taasisi mbalimbali na sekta binafsi hivyo kumwezesha mwajiriwa awapo katika eneo la kazi kufanya shughuli zake kwa amani.

"Katika kutekeleza jukumu letu la kulipa fidia kwa wafanyakazi, mfuko una kazi kubwa ya kujenga mifumo ya kutuwezesha kutoa huduma, lakini tunaamini mifumo pekee yake haiwezi na ndio maana tunawafanyakazi wenye weledi kwa ajili ya kutoa huduma hivyo tuna imani mkiwezeshwa itarahisisha Taasisi kutoa huduma bora pamoja na waajiri kuzifikia huduma zetu kwa urahisi" alisema Bw. Anslem

Ameongeza kuwa changamoto kubwa walizokuwa wakizipata ni ukosefu wa usahihi wa taarifa za majanga kutoka kwa waajiri kwenda Jeshi la Polisi na kusababisha usheleweshwaji wa kulipa fidia kwa wafanyakazi.

“Tunashirikiana na Jeshi la Polisi na haya ni maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kuzitaka Taasisi za Umma kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha tunatoa huduma kwa ufanisi kwa wananchi na ndio jukumu kubwa la Taasisi za Umma, kuwa kwetu hapa pamoja na Jeshi la Polisi ni maelekezo mahsusi kabisa ya Serikali yetu ya Awamu ya Sita, ambayo imetoa kipaumbele kuhakikisha kuwa hakuna kero hata moja kwa mwananchi ambayo haishughulikiwi kwa wakati”. alisema Bw. Anslem

Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbroad Mutafungwa amesema wao wanahusika moja kwa moja katika upelelezi, uchunguzi wa taarifa zote za wafanyakazi ambazo zimeripotiwa kwenye vituo mbalimbali vya polisi na kuzichunguza na kuwasilisha ripoti inayosaidia mfanyakazi aliyeumia kazini kulipwa fidia na WCF.

"Tunawahimiza sana waajiri kuweka kumbukumbu nzuri za wafanyakazi pamoja na kuhakikisha mnawasaidia kutoa taarifa pale wanapokumbwa namatukio ya ajali" alisisitiza Mutafungwa

Amesema waajiri walioshiriki semina hiyo wamepata elimu itakayowasaidia kubadilisha mtizamo wa wafanyakazi hususani kutambua kwamba hata kama tatizo ni dogo lazima lilipotiwe polisi ili waweze kupata haki zao kwa wakati.

Naye Lawrence Ndagula ambaye ni mmoja wa washiriki wa semina hiyo kutoka kampuni ya Mwanza Huduma amesema elimu waliyoipata itawasaidia kujua umuhimu wa kupeleka taarifa polisi pindi mfanyakazi anapopata ajali akiwa kazini.

Kwa upande wake Afisa Rasirimaliwatu kutoka kampuni ya Fluiconnecto, Azza Azzuna amesema semina hiyo imemwongezea wigo mpana wa kuwasaidia wafanyakazi wake kupata stahiki zao pindi wanaumia wakiwa kazini.

Tanzania Census 2022