ZAIDI YA TANI 5,000 ZA CHAI KUCHAKATWA NA KIWANDA CHA KISASA CHA CHAI MPONDE

News Image

Imewekwa: 16th Aug, 2022

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Profesa Joyce Ndalichako amesema Kiwanda cha Chai Mponde kinakwenda kuwa kiwanda cha kisasa ambapo kitaweza kuchakata zaidi ya tani 5,000 za chai.
Akizungumza na wadau wa Kiwanda hicho, Waziri Ndalichako alipotembelea kiwanda cha Chai Mponde kilichoko Bumbuli, Wilaya ya Lushoto Mkoani Tanga amesema Serikali imekusudia kunufaisha wakulima wa Chai zaidi na kukuza biashara nchini.
“Kiwanda cha Chai cha Mponde ni kiwanda cha Kisasa ambacho kwa siku wakulima wataweza kuuza takribani kilo elfu 50,000 na kwa fursa hiyo ya biashara itachangia nyanyua Halmashauri yetu ya Bumbuli na kuboresha maisha ya wananchi.” amesema, Mhe. Prof. Ndalichako.
Waziri Ndalichako amewafahamisha wakulima wa zao hilo kwamba amepokea maelezo na amefanya ukaguzi kwenye eneo la kupokelea na kuchambua Chai, eneo la kuichakata (Processing), eneo la kuangalia viwango na ubora (Grading), eneo la Karakana, Tanuri la kufua joto(Boiler) na kote huko kumekamilika na hivyo kujiridhisha kuwa kiwanda kimekamilika kwa asilimia 95%.
Waziri Ndalichako pia amesema Wizara yake tayari imekutana na Watendaji Wakuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) pamoja na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ambao ndio wawekezaji wakuu kwenye kiwanda hicho na kuona namna bora ya kukamilisha sehemu ndogo iliyobakia ili Kiwanda kianze shughuli zake za uzalishaji mara moja .
“Kulikuwa na baadhi ya vifaa ikiwemo mabomba ya kutolea mvuke na nyavu za kukaushia chai ambavyo vilihitajika ili kukamilisha hatua za uzalishaji.” Alifafanua.
Katika ziara hiyo Mhe. Profesa Ndalichako alifuatana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Omary Mgumba, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Mhe. Kalist Lazaro, Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dkt. John Mduma, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, Bw. Marco Kapinga, Mwenyekiti wa Bodi ya Kiwanda hicho, Bw. Anselim Peter, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Bw. Nichodemus Mauya na watendaji wengine wa kiwanda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba amesema tangu kiwanda kilipofungwa mwaka 2013, uchumi wa Halmashauri hii umedumaa na ushahidi ni mapato ya Halmashauri.
“Sisi watu wa Lushoto na hasa Bumbuli, uchumi wetu mkubwa unategemea Chai, nawahimiza ndugu zangu wakulima wa Chai kuanza uzalishaji wa zao hilo kwa wakati kwani kiwanda kitaanza kazi mapema kama ambavyo Serikali imeelekeza” Alisema.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WCF Dr. John Mduma amemhakikishia Mhe. Waziri Prof. Ndalichako kuwa maelekezo yatatekelezwa ipasavyo ili kuhakikisha kiwanda kinafanya kazi kama ilivyopangwa.
Nao wakulima wa Chai wameonyesha matumaini makubwa kufuatia ziara ya Waziri Ndalichako ambapo baadhi yao walifuatana nae katika kukagua maendeleo ya kiwanda hicho.
“Tumeona mabadiliko makubwa yamefanyika, nimshukuru sana Mhe. Rais wetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa hii iliyofanyika.” alisema mmoja wa wakulima wa Chai Bumbuli Mzee Said Ngereza.
Waziri Ndalichako amefanya ziara hiyo Agosti 16, 2022, ikiwa ni siku sita tu baada ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Komredi Daniel Chongolo kuzungumzia umuhimu wa Kiwanda hicho kwa wakulima na kukuza biashara na uchumi wa nchi yetu.
Kiwanda cha Chai cha Mponde ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ya Awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kuwanyanyua wakulima na kukuza biashara nchini.