RAIS AJIVUNIA HUDUMA ZA WCF KWA WANANCHI-LULIDA

News Image

Imewekwa: 28th Oct, 2023

WAJUMBE wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, wameridhishwa na huduma zitolewazo na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) baada ya kusikilzia ushuhuda wa baadhi ya wanufaika wa fidia wakati wa ziara ya Kamati ya kutembelea ofisi za Mfuko huo jijini Dar es Salaam Oktoba 28, 2023.

Wajumbe hao walioongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Riziki Lulida, walipata fursa ya kupata maelezo ya utekelezaji wa shughuli za Mfuko kutoka kwa watendaji wa Mfuko, kabla ya kusikiliza ushuhuda

“Niwapongeze WCF kwa kazi kubwa na nzuri mnayoifanya, nitapeleka salamu kwa Mhe. Rais ambaye amekuwa mstari wa mbele kusaidia makundi mbalimbali yakiwemo ya wanawake, Vijana na wenye ulemavu,na hili mnalofanya mnamfanya ajivunie huduma mnazotoa kwa wananchi.” Alisema Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mhe. Riziki Lulida.

Naye Mhe. Katani Ahmed Katani, yeye amepongeza huduma za WCF ambazo kwa kiasi kikubwa zimekuwa faraja kwa wafanyakazi wanaoumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi.

“Kwa sababu mnaenda vizuri ni matarajio yetu wanaopata ajali au magonjwa kazini, ninyi ndio mtakaowafuta machozi."Alisema.

Aidha, Wajumbe hao walishauri kufanyiwe marekebisho ya Sheria kuhusu ukomo wa kuwasilisha madai kwa mtu anayeumia kutokana na ajali ambapo Sheria iliyopo imeweka ukomo wa miezi 12.

"Jambo hili ningeshauri lifanyiwe marekebisho, ili kwa mtu aliyechelewa kuwasilisha taarifa kutokana na sababu mbalimbali, aweze kuruhusiwa kuwasilisha madai na hapa atakuwa amepata haki yake." Alishauri Mhe. Michael Kembeki.

Bi. Ester John, yeye ni mnufaika wa fidia kama mtegemezi, mumewe ambaye alikuwa mtumishi wa Hospitali ya Wilaya ya Chunya Mkoani Mbeya, alifariki katika ajali ya gari wakati akitekeleza majukumu ya mwajiri wake.

“Wakati tunampoteza mpendwa wetu, mimi nilikuwa ugenini, sina ndugu yoyote nilifanyiwa operesheni ya uzazi, WCF, ilitusaidia, Mafao ya kila mwezi ninayoyapokea yanasaidia kuendesha maisha yangu mimi pamoja na mtoto.” Alisema.

Mnufaika mwingine, Bw. Hassan Jambau, yeye aliwaambia wajumbe hao kuwa tangu alipoumia hadi kupona na kubaki mlemavu wa mguu, WCF imekuwa pamoja naye.

“Sina mengi ya kusema, zaidi ya kutoa shukrani nyingi kwa WCF.” Alisema.

Bw. Kelvin Mwemezi, ambaye naye aliumia mguu baada ya kuchomwa na kitu chenye ncha kali, alisema, Mfuko umekuwa msaada mkubwa na umekuwa kama sehemu ya familia yake baada yay eye mwenyewe kupoteza wazazi wake.

“Namshukuru sana Mheshumiwa Rais, kwa kuanzisha Mfuko huu, nawashukuru sana ninyi viongozi na wafanyakazi wa WCF, nilikuwa nimekata tama ya maisha baada ya kuumia, na mama yangu kufariki, lakini Mfuko umenifuta machozi.” Alisema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemabvu), Mhe. Patrobas Katambi, aliwashukuru wajumbe wa Kamati hiyo kwa kutembelea WCF ambayo iko chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu.

“Napenda kumshukuru sana Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye yeye ndiye ametuwezesha kwa kutupatia vitendea kazi ambavyo vinatusaidia kutekelza majukumu ya kulipa fidia kama mlivyopata ushuhuda hapa.” Alisema.

Aidha, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Mhandisi, Cyprian Luhemeja, amesema kwaniaba ya Serikali, wamepokea ushauri na mapendekezo yaliyotolewa na wajumbe ili kuhakikisha kazi nzuri inayofanywa na Mfuko ya kuhudumia watanzania inakuwa bora zaidi.

"Tutajaribu kuangalia yale yanayowezekana kubadilishwa kisera tutayarekebisha na Yale yanayohusiana na convations za ILO nazo tutajaribu kuangalia namna nzuri ya kutekeleza majukumu yetu." Alisema Mhanisi Luhemeja.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa WCF, Dkt. John Mduma amesema, WCF imeendelea kujenga mifumo ya kufanyia kazi ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wanachama.

“Zaidi ya asilimia 90 ya huduma zinapatikana kwa njia ya mtandao.” Alifafanua.