WCF yafanya mafunzo kwa Viongozi wa TUICO

News Image

Imewekwa: 27th May, 2019

Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF) amewataka viongozi wa Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO) kutoa elimu ya fidia ili kufikisha ujumbe kwa wanachama walengwa.

Mkurugenzi wa Uendeshaji, Bw. Anselim Peter alitoa wito huo kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, Bw. Masha Mshomba wakati akifungua mafunzo ya siku moja ya Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa viongozi wa TUICO ngazi ya Taifa na Makatibu wa Mikoa yaliyofanyika katika Ukumbi Wa Mikutano wa NSSF Morogoro, tarehe 24 Mei 2019.

“Ninaamini kuwa TUICO kwa nafasi yenu mtakua wawakilishi wazuri ili kuhakikisha kila mfanyakazi anaufahamu na kuulewa ipasavyo Mfuko huu. Hii ni fursa nzuri kwa kuwa nina imani baada ya mafunzo haya mtakuwa wawakilishi wazuri kwa wanachama wa TUICO waliopo katika matawi yenu. Ni wazi mtawatembelea na kuwapa elimu mliyoipata”, alisema Bw. Peter na kuongeza;

“Haya ni maeneo muhimu kwenu kuyafahamu kwa kuwa kama viongozi wa chama, licha ya kuwa wadau wakuu katika Mfuko lakini pia mnasimamia mahusiano baina ya mwajiri na mfanyakazi katika kulinda haki na kutetea maslahi ya wafanyakazi ambao ndio wanachama wa TUICO”.

Mafunzo hayo ni utekelezaji wa mpango mkakati wa Mfuko kwa mwaka 2018/19 wa kutoa elimu kwa Wadau mbalimbali na miongoni mwa Wadau hao ni Vyama vya Wafanyakazi. “Hii ni fursa nzuri kwa kuwa nina imani baada ya mafunzo haya mtakuwa wawakilishi wazuri kwa wanachama wa TUICO waliopo katika matawi yenu. Ni wazi mtawatembelea na kuwapa elimu mliyoipata”, alisema Bw. Peter.

Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Katibu Mkuu wa TUICO, Bw. Boniface Y. Nkakatisi aliushukuru Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi kwa mafunzo hayo ambayo watayatumia kufikisha ujumbe kwa wanachama wao.

“Niwashukuru sana watoa mada kwa maelezo ambayo wameyatoa kwetu. Tumeelewa maarifa yote ambayo wametupa na tunapenda kuwaahidi kuwa tutayafanyia kazi kama ilivyokusudiwa. Elimu tuliyopata tutakwenda kuwaeleza wanachama wetu”.

”Semina hii ina manufaa sana kwetu na tunaomba huu usiwe mwisho wa kupeana elimu hii. Tunaomba mkubali mialiko ya mikutano yetu ili Taarifa na maarifa haya yajulikane kwa wanachama wetu wote na wananchi kwa ujumla”, alisema Bw. Nkakatisi.

Mafunzo hayo ya siku moja yalilenga kuwapa uelewa viongozi wa TUICO kuhusu Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi hususan katika kufahamu madhumuni ya kuanzishwa kwa Mfuko, wajibu na haki za waajiri na wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria ya Fidia, kufahamu namna ya usajili na uwasilishaji wa michango na uwasilishaji wa madai na kufahamu taratibu za ufanyaji wa tathmini na ulipaji wa Fidia.