Mafao

ULIPAJI WA FIDIA

Fidia ni malipo au huduma inayotolewa kwa mfanyakazi au wategemezi wa mfanyakazi baada ya mfanyakazi kupata ajali, ugonjwa ama kufariki kutokana na kazi aliyoajiriwa nayo.

Ulipaji wa Mafao ya fidia unahusisha matukio ya ajali, ugonjwa au kifo yaliyotokea kuanzia Tarehe 01 Julai 2016 na kuendelea. Aidha, madai ya fidia yanapaswa kuwasilishwa ndani ya kipindi kisichozidi miezi kumi na mbili (12) tokea tukio husika lilipotokea au kugundulika.

Malipo ya fidia yanaweza kulipwa kwa malipo ya vipindi maalum (Periodical payments), malipo ya mkupuo (Lumpsum) na Pensheni ya kila mwezi kulingana na aina ya ulemavu, asilimia ya ulemavu na kiwango cha utegemezi

Aidha wafanyakazi wote walioumia, kuugua ama kufariki kutokana na kazi kabla ya Tarehe 01 Julai 2016, madai yao yatashughulikiwa kwa utaratibu na kwa mujibu wa Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi ya Mwaka 1949 na Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya Mwaka 2002.

Mfuko unatoa mafao yafuatayo;

a)Huduma ya matibabu

b)Malipo ya ulemavu wa muda

c)Malipo ya ulemavu wa kudumu

d)Malipo kwa anayemhudumia mgonjwa

e)Huduma za utengemao

f)Msaada wa mazishi

g)Malipo kwa wategemezi endapo mfanyakazi atafariki.

WALENGWA WA MAFAO

Walengwa wa Mafao yanayotolewa na Mfuko ni:

a)Wafanyakazi ambao wataumia au kuugua kutokana na kazi waanazozifanya kwa mujibu wa mikataba ya ajira zao.

b)Wategemezi wa mfanyakazi atakayefariki kutokana na ajali au ugonjwa uliotokana na kazi.

VIGEZO VYA KULIPA FIDIA

Miongoni mwa vigezo vinavyozingatiwa na Mfuko wakati wa kulipa fidia ni pamoja na;

a)Kama ajali, ugonjwa ama kifo kilitokea wakati mwajiriwa akitekeleza majukumu yake au kilitokana na kazi yake;

b)Kama mfanyakazi amepata ulemavu, ugonjwa au amefariki kutokana na kazi;

c)Kama hakukuwa na vitendo vya jinai kinyume na sheria vilivyofanywa kwa makusudi na mwajiriwa na vikampelekea kupata ajali ama kifo (willful misconduct);

d)Michango yote iwe imelipwa;

e)Nyaraka zinazohusu tukio husika zimewasilishwa.